Featured Posts

test

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, March 18, 2014

FURAHA YA BABU SEYA NA PAPII YAANZA UPYA. WAKILI ANASA USHAHIDI WA KUWATOA GEREZANI.Na Elvan Stambuli na Haruni Sanchawa

MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ anayetumikia kifungo cha maisha jela na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kwa kuwanajisi watoto tisa, wana furaha upya baada ya mwanga wa kuweza kurudi uraiani kuchomoza tena, wakili wao, Mabere Nyaucho Marando amezungumza na Uwazi.

KASORO HUKUMU YA MWANZO Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Marando alisema kwamba katika kesi ya Babu Seya na mwanaye iliyosikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar aligundua kuna vielelezo muhimu ambavyo havikuambatanishwa hivyo kuwa vigumu kwake kuviingiza na kuvitetea katika ngazi ya mahakama ya rufaa iliyoshindilia adhabu dhidi ya wawili hao.

Marando alisema mwanga mwingine wa kupitiwa upya wa mashitaka yao umekuja baada ya kuwepo kwa kesi mpya inayofanana na ya akina Babu Seya kwa asilimia mia moja. Alisema kesi hiyo ipo kwenye hatua ya mwisho ambapo ushindi wake utamfanya apate nguvu ya kurudi mahakamani kuwatetea wafungwa hao waliohukumiwa mwaka 2004.

DIRA KWENYE KESI HIYO “Kuna kesi mahakama kuu kanda moja nchini inayotetewa na wakili maarufu (jina tunalo). Hii kesi inafanana sana na ya akina Babu Seya. Uzuri wake ina dalili zote za washtakiwa kuibuka na ushindi wa kishindo. MAHOJIANO Mazungumzo kati ya Marando na Uwazi yalikuwa hivi:

Uwazi: Lakini mheshimiwa kesi ya Babu Seya si ilifika katika rufaa mara tatu na wakashindwa na ulisema hakuna namna tena, sasa itakuwaje kurejeshwa tena huko? Marando: Ni kweli, lakini ni jambo linalowezekana.

Nimesema kama hiyo kesi ninayoitaja watashinda na wanaweza kushinda, basi mimi nitaenda kwa Nguza na kumwambia wazo langu, akikubali nitaiandikia barua mahakama ya rufaa kuomba kupitiwa tena kwa yale mashitaka, nitajenga hoja.

Uwazi: Hiyo kesi unayoingoja hukumu yake inahusu nini? Marando: Inahusu kubaka na kulawiti, ni kama hii ya Babu Seya na wanawe. Hakuna tofauti. Sasa washitakiwa wale wakishinda ndipo hoja inapokuja, kwa nini vipengele vilevile viwatie hatiani akina Babu Seya wengine viwaweke huru, ndivyo inavyokuwa katika kesi. Uwazi: Ukiwaandikia mahakama ya rufaa wakakubali, majaji walewale watasikiliza ombi lako?

Marando: Hilo ni la mahakama lakini idadi inaweza kuongezwa na kufikia majaji sita au saba.Uwazi: Una hakika utashinda na kukubaliwa? Marando: Kama nilivyokueleza, ikipita ile kesi halafu mahakama ya rufaa wakakubali kupitia tena jalada, nina uhakika wa kushinda.

ANALIPWA NA NANI? Wakili huyo maarufu alisema yeye aliwatetea wanamuziki hao bure kwenye kesi yao ikiwa katika ngazi ya mahakama ya rufaa baada ya kusoma jalada lenye kurasa 1,362 ambapo aligundua kuwa kuna nyaraka kadhaa ambazo hazikuambatanishwa katika Mahakama ya Kisutu ambazo zingeweza kuwaokoa na kifungo wateja wake.

“Unajua kesi inapokuwa mahakama ya rufaa, majaji wanachofanya ni kupitia jalada si kusikiliza, hivyo haiwezekani kuambatanisha vielelezo vipya,” alisema Marando ambaye anajipambanua kuwa awali alishinda nusu kwa kuwatoa nje watoto wa Babu Seya, Mbangu na Francis Nguza ambao nao walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa moja na wafungwa hao.

HUKO NYUMA Juni 25, 2004 Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya aliwatia hatiani kwa ubakaji na ulawiti Babu Seya na wanawe Papii Kocha, Mbangu na Francis. Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu hiyo.

Wakili Marando akapeleka suala hilo Mahakama ya Rufaa Tanzania ambako Mbangu na Francis waliachiwa huru na yeye kutangaza kwamba ameshinda nusu. Babu Seya na wanawe walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka na kulawiti watoto hao kati ya Aprili na Oktoba 2003 katika maeneo ya Sinza ya Kwaremmy, Dar es Salaam.
GPL

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages