Featured Posts

test

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, November 11, 2014

SITTI MTEMVU KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UDANGANYIFU.

Huku akiwa ametangaza kuvua taji la urembo la Taifa 'Redd's Miss Tanzania 2014', Sitti Mtemvu, anadaiwa kuandaliwa hati ya mashtaka kuhusiana na tuhuma za kudanganya umri wake ili kutimiza sifa za kushiriki shindano hilo ambalo fainali zake kitaifa zilifanyika Oktoba 11, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari NIPASHE ilizozipata jijini jana zinadai kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) tayari wameshabaini kwamba Sitti alipata cheti kipya kwa njia ya udanganyifu na sasa wanaendelea kuchunguza ili kuwabaini wale waliohusika katika kukipata cheti hicho ili wote waweze kushtakiwa pamoja.

Chanzo chetu kiliendelea kueleza kwamba taasisi hiyo imechukizwa na sakata hilo na inataka kuchukua hatua zinazostahili ili iwe fundisho kwa wote ambao wanania ya kufanya kosa la aina hiyo.

"Imebainika kuwa watu wengi wanatoa taarifa zisizo sahihi ili kupata vyeti vipya vya kuzaliwa kwa lengo la kuwasaidia katika kupata ajira, nafasi za masomo au kurahisisha mambo yao mengine, sasa hatutaki taasisi yetu iendelee kuchafuliwa jina, kuna tamko litatolewa hivi karibuni, hatutakaa kimya," kiliongeza chanzo chetu.

WANASHERIA WALONGA
Alex Mgongolwa, wa jijini aliliambia gazeti hili kuwa kosa la kughushi limegawanyika katika sehemu mbili na kila moja lina adhabu yake tofauti.

Mgongolwa alisema kuwa kosa la kwanza la kughushi nyaraka adhabu yake ni miaka saba jela kama ilivyoainishwa katika kifungu cha kanuni cha adhabu namba 333.

Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, alisema katika kifungu cha 337 endapo mtu atapatikana na hatia ya kutumia hati iliyoghushiwa, hukumu yake itakuwa ni kwenda jela kwa muda wa miaka mitatu.

"Kama mtuhumiwa atakuwa amekutwa na hati hiyo ya kughushi na alishiriki pia katika kuitengeneza atakumbana na adhabu zote mbili," alisema mwanasheria huyo maarufu na mwanachama wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katibu Mkuu wa zamani wa Simba na aliyekuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Sheria wa TFF, Evodius Mtawala, alisema kuwa kifungu cha 339 kinaeleza kwamba mtu atakayebainika amedanganya kwa kughushi atatakiwa kwenda jela kwa muda wa miaka saba.

"Ila kifungu cha 338 ambacho kinaeleza makosa ya kughushi wosia, hati za ardhi, hukumu ya mahakama, hundi, nyaraka za benki, fedha au malipo yoyote, adhabu yake ni kifungo cha maisha," alisema Mtawala.

Naye Wakili, Damas Ndumbaro, alisema kuwa kwanza mtu atakayebainika na kosa hilo anatakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja na hukumu yake itatolewa ya kwenda jela na haina faini.

"Uthibitisho ukishapatikana mtu huyo anafikishwa mahakamani moja kwa moja," Ndumbaro aliongeza.Kifungu namba 28 (3) cha Sheria ya Kuandikisha Vizazi na Vifo ya Rita kimeweka wazi kuwa atakayebainika ametoa taarifa za uongo ili kupata cheti cha kuzaliwa adhabu yake ni kwenda jela kwa muda usiopungua miaka mitatu. 

Cheti ambacho Rita inakifanyia uchunguzi ni kile kilichotolewa Septemba 9, mwaka huu chenye namba 1000580309 ambacho kinataja jina la baba wa Sitti ni Abbas Mtemvu Zuberi (Mbunge-Temeke) na mama yake ni Mariam Nassor Juma ambaye ni diwani wa Temeke, jijini Dar es Salaam.

Cheti hicho kinaonesha Sitti amezaliwa Mei 31, 1991.Moja ya taarifa za awali zilizoonekana kwenye mitandao ya kijamii siku moja baada ya mrembo huyo kushinda taji ni hati ya kusafiria inayoonesha ilitolewa Februari 15, 2007 na muda wake wa kutumika mwisho ukiwa ni Februari 14, 2017, huku zikitaja tarehe ya kuzaliwa Sitti ni Mei 31, 1989.

CHANZO:NIPASHE

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages